Ads

MAPITIO YA TAARIFA NA MATUKIO MBALIMBALI YA WIKI 19-25/FEBRUARY, 2017




Hii ni wiki ya Tatu sasa kukuletea mukhtasari wa majumuisho ya mapitio ya taarifa na matukio na misimamo ya Chama juu ya masuala mbalimbali yaliyojitokeza kuhusiana na CUF kwa lengo la kuwajulisha wanachama, viongozi na watanzania kwa ujumla masuala yepi muhimu yanayoendelea ndani ya CUF na kuwekana sawa kwa kuwapa “updates” aidha kusahihisha taarifa za upotoshwaji/propaganda chafu dhidi ya Chama (CUF Weekly Reports).

KURUGENZI YA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA WIKI HII IMEPOKEA NA KUWALETEA TAARIFA ZIFUATAZO:

1. KATIBU MKUU, MAALIM SEIF SHARI HAMAD AMEKAMILISHA ZIARA YA KIKAZI KISIWANI, PEMBA ILIYOPATA MAFANIKIO MAKUBWA;

Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, amekamilisha ziara ya siku kumi kisiwani Pemba iliyoanza tarehe 15/2/2017 na kuhitimishwa tarehe 24/2/2017 kwa kuendelea kupata mapokezi makubwa ya heshima na yaliyojaa mapenzi makubwa kwake binafsi na kwa Chama. Maalim Seif amezitembelea wilaya zote nne za kisiwa hicho ikiwemo wilaya ya Mkoani, Chakechake, Wete na Micheweni.  Ziara hiyo iliyokuwa na mafanikio makubwa na Kuimarisha Chama aliweza kufungua ofisi mpya za Chama 14, kuweka mawe ya msingi ya ofisi za chama 9, ufunguzi wa matawi mapya ya wanachama 23, na alizindua wataratibu 1489 kwa wilaya zote na kuzungumza na viongozi wa chama na Jumuiya zake. sehemu zote alizotembelea alipokewa na mamia ya wananchi wenye furaha na hamasa kubwa, Huku akipewa zawadi mbali mbali kila alipokwenda ikiwemo Ngombe, Mbuzi, Kondoo, Kuku,  Mayai, Ndizi, Maembe, Shokishoki, Halua, Asali, Mikoba ya Ukili kwa ajili ya Bi Awena, Pweza, Kanzu, Seruni, viatu na vingi venginevyo ikiwa ni ishara ya mapenzi waliyonayo wananchi juu yake. Akiwa katika Jimbo la Tumbe ameweza kuzindua rasmi Jengo la Ofisi na Ukumbi wa Mikutano wa kisasa uliopewa Jina la mama yetu BI AWENA CONFERENCE CENTER-BCC, jengo hilo lililogharimu kiasi cha shilingi 70,159,400/- zilizotokana na nguvu za wa wanachama pamoja na mchango mkubwa na Mbunge wa jimbo la Tumbe Mh. Rashid Abdallah.  Katika hatua nyingine Katibu Mkuu aliwapokea wanachama wapya kadhaa wa CCM waliokuwa viongozi wa CCM. Wanachama hao wamesema hakuna faida ya maendeleo ya kiuchumi  wala kisiasa wanayoyaona ndani ya CCM zaidi ya kupandikizwa kwa chuki na ubaguzi wa kimatabaka usiokua na maana.


Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mh.Salim Bimani katika salamu zake kwa wanachama na viongozi amehimiza “Umoja na mshikamano hasa katika kipindi hiki Chama chetu kinapita katika wakati mgumu wa kuandamwa na maadui wengi wa nje na ndani, amesema hii ni hali ya mpito tu na tutambue kwamba siku zote mti wenye matunda ndio unaotupiwa mawe, na maadui wanafanya hivi kwa makusudi kwasababu wanaona Chama cha Wananchi CUF kina dhamira yakweli, malengo ya kweli na nia ya kweli ya ukombozi katika nchi hii"  Mh.Bimani alitolea mfano kwa wasaliti na maadui wote wa Chama kwa kusema “Chama cha Wananchi

CUF nikama jiwe ukiliangukia litakujeruhi na likikuangukia litakuathiri zaidi" awamu inayofuata itakuwa ni shughuli maalumu ya kuwakabidhi wanachama wapya 7000 wa CCM ambao wamejiorodhesha kurejesha kadi zao na kupandisha bendera za waratibu.

Katibu Mkuu, Maalim Seif amewahakikishia wananchi, wanachama na viongozi wa CUF waliojitokeza kumpokea na kupata fursa ya kuzungumza nao takribani maeneo yote kwamba " Watembee kifua mbele wala wasiwe wanyonge kwani haki yao ya maamuzi waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 ipo karibu kupatikana na hakuna wakuizuia”   Katibu Mkuu aliyeambatana katika ziara hiyo na Kaimu Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar Mhe Salim
Bimani, Viongozi wengine walioambatana na Katibu Mkuu katika ziara hiyo ni pamoja na  Mhe. Said Ally Mbaruku- Mratibu wa CUF Pemba,

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi Mhe. Umar Ali Sheikh, Naibu Mkurugenzi wa fedha na Uchumi Abdallah Bakari Hassan, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe Yusuf Salim, Naibu Katibu JUKECUF Taifa Zahra Ali Hamad,  JUVICUF iliwakilishwa na Faki Suleiman, JUZECUF iliwakilishwa na Maalim Hamad, Mhe Hamad Masoud  na Mhe. Abubakar Khamisi, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa,   na viongozi wengine mbalimbali kutoka Unguja Bibi Arafa Musa uredi, Bibi Hasina Matar, Ali Salim Khamis(MB) –Mwanakwerekwe, Mbunge wa Nungwi Mhe. Miza Pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani, na wajumbe wa Baraza Kuu La Uongozi Taifa kutokea wilaya za Pemba. Katibu Mkuu amesharejea Unguja kuendelea na majukumu mengine.

2. KUHUSU KESI  DHIDI YA MSAJILI, MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, LIPUMBA NA WENZAKE:

Kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mtungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lipumba na wenzake iliitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Mahakama Kuu tarehe 21/2/2017. Kutokana na Msimamo wa Chama katika kesi hiyo kumkataa Jaji Kihiyo kuendelea na kesi hiyo. Jaji Kihiyo amekubaliana na Hoja za mawakili wa Chama na kukubali kutoa nyaraka muhimu za kisheria zinazohitajika kwa ajili ya kuwasilisha maombi ya kufanyia mapitio (REVISION) juu ya maamuzi yake ya kukataa kujitoa. Shauri hili limepangwa kutajwa tena mahakamani hapo tarehe 22/3/2017 na halitaendelea kusikilizwa na Jaji Kihiyo mpaka Mahakama Kuu ya Rufaa itakapofanya uamuzi juu ya mapitio (Revision) ya maamuzi yaliyotolewa na Jaji Kihiyo kutaka kuendelea na kesi hiyo mbali na kukataliwa na Bodi ya wadhamini ya CUF.

PONGEZI KWA WANACHAMA WETU KUTII MAAGIZO YA CHAMA:
Tuliwaomba wanachama wetu kutohudhuria mahakamani tarehe 21/2/2017 na wito huo umezingatiwa kikamilifu. Tunawapongeza wanachama na wapenzi wote wa CUF kwa kuheshimu maelekezo ya Chama CUF Taasisi. Kwa hakika hakukuwa na kilichoendelea kama tulivyoeleza hapo awali. Hata shauri halikuitwa kwenye mahakama ya wazi (Open Court) mawakili waliitwa kwa Jaji na kutolewa maamuzi hayo tuliyoyaeleza hapo juu.

Tarehe 22/3/2017 hakutakuwa na kinachoendelea, Jaji Kihiyo Tushamalizana nae na hivyo hataendelea kusikiliza shauri hili. Maelekezo yetu ni yaleyale tusiende mahakamani. Tuendelee na majukumu yetu. Tutawajulisha lini tunahitajika mahakamani kwa kesi inayohusiana na wizi wa fedha za Ruzuku na mapitio (Revision) itakayofanyika Mahakama Kuu ya Rufaa.

KESI HII INAHUSU NINI?
Tunapenda kuwajulisha wanachama wetu na watanzania kwa ujumla kuwa SHAURI lililopo mahakamani linahusiana na kumpinga Msajili wa vyama vya siasa nchini kuingilia utendaji wa shughuli za ndani ya Chama kinyume na matakwa ya sheria. Kesi iliyopo mahakamani haijadili uhalali au uharamu wa Lipumba kudai kuwa ni Mwenyekiti, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilishamsimamisha uanachama tarehe 28/8/2016 na baadae kumvua uanachama katika kikao chake cha tarehe 27/9/2016. Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa  uliofanyika tarehe 21/8/2016 uliridhia kujiuzulu kwake. Lipumba amefukuzwa uanachama akiwa mwanachama wa kawaida na si kiongozi wa nafasi yeyote katika Chama. Maamuzi ya Baraza Kuu yaliyomvua uwanachama Lipumba hayajakatiwa rufaa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa kwa mujibu wa katiba ya CUF. Hivyo, maamuzi ya Baraza Kuu ya kumvua uwanachama wa CUF yataendelea kubaki pale pale. Kwa mujibu wa katiba ya CUF, Uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi unakatiwa rufaa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa, na maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Taifa ndio ya mwisho. Na baada ya hapo asiyeridhika anaweza kwenda kupinga maamuzi hayo ya Mkutano Mkuu wa Taifa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania ibara ya 107A (1) inasema  kuwa chombo cha mwisho katika utoaji wa haki nchini ni Mahakama. Mtu yeyote asiporidhika na maamuzi ya Mahakama Kuu atakata rufani mbele ya Mahakama Kuu ya Rufaa- Tanzania na hiyo ndio ngazi ya mwisho nchini. Lipumba alipaswa kufuata njia hiyo na wala si vinginevyo.

Bahati mbaya Lipumba hajayakatia Rufaa maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mamlaka inayostahiki, yeye amekatia rufaa maamuzi hayo kwa Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi ambapo ni kinyume na katiba ya CUF. Aidha, wapo wanachama ambao Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliwasimamisha uanachama na wao kukatia Rufaa maamuzi hayo kwa Mkutano Mkuu wa Taifa, hatua za kikatiba zitazingatiwa kushughulikia suala hilo. Chama cha CUF kipo imara na uongozi upo madhubuti. Tuendelee kuwa pamoja na viongozi wa Chama na kuheshimu maagizo mbalimbali yatakayoendelea kutolewa kukabiliana na udhia huu wa Lipumba na mashabiki wake.

3. KUHUSU BODI YA WADHAMINI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI):
Kuhusu “The Registered Trustees of The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi)” Bodi ya Wadhamini ya CUF tulitoa maelezo ya kutosha wiki iliyopita. Maelezo hayo ndiyo sahihi na yataendelea kubaki hivyo yalivyo. Wajumbe 6 kati ya 9 wa Bodi ya wadhamini wapo pamoja na wanapinga kinachofanywa na Lipumba na genge lake. Mzee Yohana Mbelwa aliyetajwa kuwaunga mkono Lipumba na wenzake taarifa hizo za kweli. Wajumbe wa bodi wanaowaunga mkono ni watatu. Thomas Malima si mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya CUF. Hatambuliki na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo ndio lenye mamlaka kikatiba na kisheria kuwaidhinisha wajumbe hao. Ikiwa wanayoyasema ni kweli kwanini wanampigia simu Mzee Mbelwa za kumtukana na kumtishia usalama wake na kukusudia kumshambulia? Mawasiliano hayo ya simu yamerikodiwa na hatua stahiki zimechukuliwa dhidi ya Thomas Malima aliyehusiaka na uhuni huo. Tunastaajabu leo kuilamu Benki ambayo ilifanikisha wizi walioufanya wa Tshs. 369 milioni, Bodi ya Wadhamini ya CUF imetekeleza wajibu wake kisheria na kukomesha aina ya wizi huo waliotaka kuufanya kwa mara nyingine. Wasichofahamu na kujichanganya ‘Mungiki’ ni kwamba hawajui kuwa kuna tofauti kati ya ‘Body of Trustees and Registered Trustees’ In company law, term “perpetual succession” defined very clear that is the continuation of a corporation's or other organization's existence despite the death, bankruptcy, insanity, change in membership or an exit from the business of any owner or member, or any transfer of stock, etc. Ni kwa msingi huu hata kama kuna wajumbe wengine wa bodi watapatwa na ugonjwa wa akili (wendawazimu)  bodi inaendelea kuwa hai.

4. WANACHAMA NA VIONGOZI WA KIBITI WAPINGA KAULI ZA LIPUMBA;

Wiki iliyopita Lipumba na wafuasi wake walikusanyana na kwenda kuwahutubia wilayani Kibiti/Rufiji; Lipumba alitoa kauli za upotoshaji juu ya kujiuzulu kwake na masuala kadhaa, wanachama na viongozi wengi waliohudhuria katika kikao hicho kwa lengo la kumsikiliza wamehoji, kwanini hakuwasilisha tofauti alizozisema na Katibu Mkuu wake kama kweli kwa vikao vya Chama ili kama kuna tatizo liweze kushughulikia kikatiba kwa kutumia vikao vya Chama? Leo anadai kurejea katika Chama je Katibu Mkuu amebadilika au yupo yuleyule? Atawezaje kufanya kazi na mtu ambaye anamtuhumu kiasi hiki? Suluhu anayodai kuitaka ni ipi au anafanya usaniii wa kisiasa? Viongozi wamehoji hizo Bilioni 10 anazodai Maalim Seif kupewa ziliingizwa katika akaunti ya Chama au Binafsi? Uwapi ushahidi wa hilo? Chama kuazimia kutoweka mgombea wa Urais na kwamba Chama hakikuwa na rasilimali za kutosha kuweza kugharamia uchaguzi ndiyo siri zilizokuwa zinatolewa kama anavyodai? Wanachama na viongozi waliozungumza na kurugenzi ya habari wameeleza kusikitishwa kwao kwa Lipumba kuonekana wazi kuwa amepoteza muelekeo wa kisiasa na badala yake inaonekana kutumika Mubashara na CCM kutaka kukiyumbisha Chama na wanachama.  Viongozi wa wilaya ya Rufiji na kibiti wamemtaka Katibu Mkuu Maalim Seif Shari Hamad kuendelea na kukilinda chama dhidi ya vibaraka wa CCM na kumuomba kufanya ziara katika wilaya zao ili kuimarisha umoja na mshikamano katika chama. Hakuna kiongozi aliokwenda kumuomba Lipumba arejee katika nafasi ya uenyekiti zaidi ya wale walewale waliomshawishi kujiuzulu wakati ule.

Katika katiba ya CUF hakuna Ibara inayozungumzia kiongozi aliyejiuzulu kuweza kutengua kujiuzulu kwake. Sio kweli kuwa mamlaka iliyomchagua haikuwa na taarifa ya kujiuzulu kwake kwa kuwa alitangaza hadharani KUNG’ATUKA katika nafasi ya uenyekiti na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida kutokana na kusutwa na dhamira na nafsi yake. Lipumba anasema wajumbe 324 waliandika barua na kupeleka malalamiko yao kwa Msajili. Lakini Msajili ameandika katika barua yake kuwa amepokea Barua iliyosainiwa na watu watatu wakiwawakilisha wajumbe 216 sasa hapa ni nani mkweli? Msajili au Lipumba? Lakini kamati ya CUF iliyoshughulikia suala hili baada ya kufanyia uhakiki majina hayo waligundua udanganyifu wa majina zaidi ya 74 yaliyojirudia na kusainiwa kwa kugushi. Kura zilizomkataa Lipumba katika Mkutano Mkuu tarehe 21/8/2016 ni 476 na wajumbe wa Mkutano Mkuu walikuwa 700. Hii inadhihirisha ni jinsi gani wajumbe wa Mkutano mkuu waliowengi walivyokuwa hawakubaliani nae kwani alijiuzulu na kukiacha chama katika kipindi kigumu cha Uchaguzi. Kosa kubwa analolifanya Lipumba ni kutaka kuaminisha wanachama na watanzania kuwa yeye ana tofautiana na Katibu Mkuu. Wakati ukweli hauko hivyo. Alipojiuzulu hakujiuzulu kumkomoa Katibu Mkuu. Yeye alikuwa kiongozi wa Chama na Mwenyekiti wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. Alipewa dhamana kubwa ya kukisimamia chama. kwanza anapaswa kuwaomba radhi wanachama, viongozi na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kama anataka suluhu aelekeze maombi yake kwa wajumbe hao ambao ndio wenye mamlaka ya kukisimamia chama sio kila siku kuzungumzia Katibu Mkuu apokei simu, Haitamsaidia.

5. UCHAGUZI MDOGO WA MITAA NA VIJIJI LINDI MJINI;
Wana-CUF wilaya ya Lindi wameendelea na Maandalizi ya uchaguzi mdogo wa mitaa saba na baadhi ya vijiji na vitongoji utakaofanyika tarehe 12/3/2017. Uandikishaji umekamilika na kampeni za uchaguzi huo zinaanza rasmi leo tarehe 26/2/2017 na CUF itazindua kampeni zake katika kata ya Mitandi mtaa wa Mnubi.  Wanachama, Wabunge na Madiwani wa maeneo mbalimbali wameombwa kujitokeza kwenda kushirikiana na viongozi wetu wa wilaya katika kampeni na kutoa michango yao ili kufanikisha ushindi kwa CUF.

6. TAARIFA YA MISIBA:
Chama chetu cha CUF kimepokea taarifa za misiba iliyotekea wiki hii ambapo; Naibu Katibu Mkuu –Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui amepata msiba wa Mama yake Mzazi Bi Maryam Mohamed Suleiman Mauly na mazishi yamefanyika jana Unguja, pia Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa Mhe Julius Mtatiro amepata misiba ya wajomba zake wawili Mkoani Mara Mzee Andrew C. Mumwi na Mzee Silyvester Korogo. Lakini pia tumepokea taarifa ya msiba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake –JUKECUF Morogoro Mjini Bi. Zainab (Zena) Mswagala kilichotokea jana na mazishi yatafanyika leo Morogoro Mjini. Aidha, Mhe. Hamidu Bobali (MB) ametutaarifu kutokea kwa mafuriko jimboni kwake Mchinga-Lindi Vijijini na kusababisha madhara makubwa na mpaka sasa wananchi wake sita wamefariki kutokana na mvua kubwa zinazoendelea. Tunawatakia wote subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Tunamuomba Mwenye-Enzi Mungu awasamehe marehemu wote mapungufu yao na awaingize katika neema za milele kwa rehema zake.  “Hakika sisi sote ni waja wa Mwenye-Enzi Mungu na kwake yeye pekee tutarejeshwa”

CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI

HAKI SAWA KWA WOTE

----------------------------------------------
MBARALA MAHARAGANDE
K/NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA- CUF TAIFA
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577

1 comment: