Ads

UHUSIANO WA TANZANIA NA CHINA UNACHOCHEA UCHUMI – MAMA SAMIA.

Displaying PIX3.jpg

Na Jacquiline Mrisho 
mwambawahabari
Uhusiano uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya watu wa china ni kichocheo kikubwa cha maendeleo baina ya pande zote mbili.

Kauli hiyo imetolewa leo na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za maadhimisho  ya mwaka mpya wa kichina zilizofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais Mhe. Samia amesema kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anatambua umuhimu wa ushirikiano huo na ameipongeza Serikali ya China kwa kuwa mshirika muhimu katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.


Miradi hiyo inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China inajumuisha Sekta za Elimu, Afya, Kilimo Ujenzi na Uchukuzi.

Ushirikiano uliopo kati ya nchi yetu na China utawezesha Tanzania kujenga viwanda ambavyo vitasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa, alisema Mhe. Samia.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania pamoja na kupambana na rushwa.

Dkt. Lu Youqing amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania kama ilivyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo.
Ni desturi kwa taifa la China kuadhimisha mwaka mpya na kuupa majina tofauti kulingana na miaka, mwaka huu wa kichina unaitwa mwaka wa Kuku Jogoo ambao hutokea kila baada ya miaka 60.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe.Charles Mwijage, jamii ya wachina waliopo Tanzania.

No comments