SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUWACHUKULIA HATUA WANAOHUJUMU MAENDELEO
Masanja Mabula -Pemba …
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imechoshwa na vitendo vya hujuma vinavyofanywa na watu wasioitakia mema Zanzibar na kuahidi kushusha kikosi kazi cha askari kutoka Jeshi la Polisi Makao Makauu ili wafanye uchunguzi na wahusika waweze kupatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria .
Imesema vitendo hivyo vinafanywa na watu kwa makusudi vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi na wananchi wake pamoja na kuhatarisha usalama , amani na utulivu wa nchi .
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili Mohammed Aboud Mohammed wakati akizungumza na wananchi katika kitalu cha miti ya matunda na misitu cha wanakikundi wa kaya maskini kilichomwa moto huko Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete usiku wa kuamkia Jumapili .
Amesema Serikali itawasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar haraka iwezekanavyo ili kikosi hicho kifike na kuanza kazi ya uchunguzi dhidi ya wahalifu wanaoendesha vitendo vys hujuma hizo .
Waziri Aboud amewataka wananchi kushirikiana na Kikosi hicho kwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitafanikisha kuwabaini wahusika na vitendo hivyo na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani .
“Kikosi kazi kutoka Jeshi la Polisi makao makuu kitatumwa haraka iwezekanavyo kufanya uchunguzi wa kina juu wa wahusika wa matukio haya , Serikali imechoshwa na hujuma za kila siku kwa sasa tumeamua kuvikomesha tunawaomba wananchi watoe ushirikiano ”alifahamisha .
Aidha Waziri Aboud amefahamisha kwamba katika hilo Serikali itakusudia kuendesha kura ya siri katika shehia hiyo ambayo itasaidia kuwaweka bayana wahusika na wanajihusika na vitendo vya kuhujumu mali za wananchi wasio kuwa na hatia .
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadidi Rashid amemweleza Waziri kuwa tayari Serikali ya Wilaya inazo taarifa za awali juu ya wahusika wa hujuma hizo na kwamba ameviagisa vikosi vya ulinzi kuhakikisha wanawakamata kwa ajili ya upelelezi .
Amesema kuwa kitalu hicho ambacho kinasimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini TASAF , ni moja ya miradi iliyoibuliwa na wananchi wenyewe ambao walikusudia kuipanda sehemu za wazi ili kurejesha uhalisia wa maeneo hayo .
Akitoa utafafanuzi , Afisa Kutoka Idara ya Misitu Pemba Assaa Sharif Ngwali amesema ndani ya kitalu hicho tayari miti mbali mbali ikiwemo miembe , Mifenesi , Mitondoo na misaji ambapo malengo ya baadaye ni kuotesha miti 22,000.
Aidha hujuma hizo pia zzilizofanywa na watu wasiojulikana wamekata kata migomba 40 ya Shufaa Assa Muombwa pamoja na shamba la Mihogo la Khamis Oma Kibano lenye ukubwa wa ekari ambapo mashsina 397 yameng’olewa
Post a Comment