SERIKALI: VIPIMO VYOTE VYA MSINGI KUPATIKANA KATIKA HOSPITALI ZA KANDA NA MIKOA.
Na Daudi Manongi
mwambawahabari
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imesema kuwa ina mkakati mkubwa wa kuhakikisha vipimo vyote muhimu vinapatikana katika Hospitali za Kanda na Mikoa nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya alipokuwa akiongea katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa ya TBC1 kwa ushirikiano na Idara ya Habari-MAELEZO.
“Mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha huduma zote ziwe karibu na wananchi na pia vipimo vyote vya msingi vipatikane mahali wananchi walipo kwa mfano tunategemea kuwe na mashine za mionzi ya X ray,Ultra sound,na vipimo vya Moyo katika hospitali za Wilaya na pia hospitali zote za kanda zitakuwa na vipimo vyote vya kirufaa,”Aliongeza Dkt Mpoki.
Aidha amesema Serikali inategemea kuweka wataalamu na vifaa katika Hospitali za Kanda na Rufaa ambapo kwa sasa kuna hospitali nne za kikanda ambazo ni KCMC, Bugando (BMC), Taasisi ya Benjamini Mkapa mkoani Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na nyingine ambayo iko katika ujenzi mkoani Mtwara na pia mkoani Tabora ambazo zote zitakuwa na vifaa na wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali iko bega kwa bega na wadau wa Afya ambapo katika Halmshauri ambazo hazina Hospitali wataingia mkataba wa huduma na Hospitali teule ikiwamo za dini na binafsi ambapo wagonjwa watapata huduma bila matatizo ili mradi wafuate sera tulizoweka pamoja na kanuni,taratibu na sheria za uendeshaji wa Taasisi hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizo Bora.
Mbali na hayo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuwa kila Kijiji kiwe na Zahanati bora ambapo kutakuwa na tabibu, muuguzi na mfanyakazi wa afya ya jamii.
Post a Comment