Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari
Kumekuwa na taarifa za upotoshwaji kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula hapa nchini ambapo hali hiyo inasababisha wananchi kukata tamaa ya kuendelea kufanya kazi hasa ya kilimo na badala yake kubaki kuilalamikia Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizebawameihakikishia nchi kuwa Tanzania iko salama na chakula kipo cha kutosha hivyo wananchi wasisikilize watu wengine ambao wana nia ya kuupotosha Umma.
Akizungumza baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alisema nchi haijakumbwa na baa la njaa na aliwataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei za vyakula.
Nae Waziri Tizeba alisema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa hali ya chakula ni mbaya.
Tatizo kubwa lililopo ambalo linawachanganya Watanzania wengi ni kuchanganya kati ya ukame na ukosefu wa chakula, wanaamini kuwa nchi ikiwa na ukame lazima kutakuwa na njaa lakini si kweli kuwa vitu hivi vinaendana.
Nchi yaweza kuwa imekumbwa na janga la ukame lakini isiwe na janga la njaa kwani kuna mazao ambayo yanastahimili ukame ambayo yanaweza yakalimwa na kutoa mazao yatakayowawezesha wananchi kujipatia chakula pamoja na kuuza ziada ya chakula hicho ili kupata fedha za kujikimu.
Mazao mengi ya jamii ya nafaka yana uwezo mkubwa wa kustahimili ukame, mazao hayo ni pamoja na mihogo, viazi na mahindi, hivyo wananchi wanapaswa kwenda na wakati kama hali ya nchi ni ya ukame basi walime mazao yanayoendana na wakati huo na si vinginevyo.
Tusiwe wabishi kung’ang’ania kufanya kilimo ambacho tumekizoea kwani hali ya hewa ama tabianchi kubadilika ni jambo lisiloepukika na linatokea muda wowote, hakuna wa kulaumiwa kuhusu mabadiliko hayo zaidi ya wananchi wenyewe kukubali mabadiliko hayo na kwenda sawa nayo.
Pia tunashauriwa kutumia mbegu zitakazokomaa mapema ili kupata mavuno kwa haraka na kwa wingi pamoja na kutumia mazao wanayoyapata kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya.
Serikali pia inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wananchi kuwa na maisha bora ambapo pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha,
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe nchini ambayo inatarajiwa kukamilika Januari 28 mwaka 2017 na itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe nchini.
Hivyo wananchi wanatakiwa wafanye kazi, wasifate maneno ya watu yenye lengo la kupotosha jamii bali wawasikilize viongozi wao ambao waliwachagua wakiamini kuwa watawaongoza na watawatatulia matatizo yao.
Post a Comment