Ads

WATUMISHI WA KARAKANA ZA TEMESA WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI.

mwambawahabari
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akizungumza na watumishi wa karakana za TEMESA wakati akifungua mafunzo kwa watumishi hao Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi wa karakana za TEMESA wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu(hayupo Pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watumishi hao Jijini Dar es Salaam.


Na Theresia Mwami TEMESA
mwambawahabari

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa karakana juu ya mfumo wa utozaji gharama za matengenezo ya magari katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za uzalishaji na matengenezo za kila mwezi.


Dkt. Mgwatu amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuleta uwiano sawa katika gharama za matengenezo ya magari kwa karakana zote za TEMESA bila kujali mikoa zilipo karakana hizo.


Aliongeza kuwa utaratibu utakaoelekezwa katika mafunzo hayo utasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ya serikali, suala linalolalamikiwa na wateja wa TEMESA kwa muda mrefu sasa.


“Nataka sasa tuanze kutoza gharama za matengenezo ya magari kulingana na muda unaotumika kutengeneza gari husika (man hour), badala ya kutumia kigezo cha asilimia ya fedha iliyotumika kununulia vipuri kwa ajili ya matengenezo ya magari, kwani baadhi ya vipuri ni ghali sana lakini hutumia muda mchache sana kuvifunga,” alisema Dkt. Mgwatu.


Dkt. Mgwatu alisema kuwa, kumekuwa na changamoto ya uwasilishaji wa taarifa za utendaji  kutoka katika mikoa/vituo vya TEMESA, mara nyingi taarifa hizi hazifiki kwa wakati. Huku akisisitiza kuwa ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo taarifa hizo zitakuwa zikifika kwa wakati tena zikiwa sahihi.


Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo, Mhandisi Sylivester Simfukwe alisema idara yake imejipanga kutoa huduma bora zinazokidhi viwango hasa katika matengenezo ya magari ya serikali, ili kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka na kero za wateja zinakwisha.
 Aliongeza kuwa mafunzo kama hayo yatatolewa kwa wawakilishi wa karakana zote za TEMESA nchi nzima.


Mafunzo hayo elekezi juu ya Mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanafanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa MT. Depot, Dar es salaam na yamehusisha watendaji wa TEMESA kutoka mikoa ya Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, pamoja na vituo vya MT. Depot na Kikosi cha Umeme.

No comments