Ads

UGATUAJI (UPELEKAJI) WA MADARAKA KWA WANANCHI WAZIDI KUIMARIKANA KUCHPCHEA MAENDELEO.



Na: Frank Shija-MAELEZO.
mwambawahabari

Yapata miaka 55 imepita ikiwa ni muda ambapo wanajeshi wa lililokuwa jeshi la Tanganyika walipojikusanya katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kushusha chini bendera ya Malkia wa Elizabeth wa Uingereza na kupandisha bendera ya Tanganyika ikiwa ni kielelezo cha kuwa sasa Tanganyika (Tanzania Bara) iko huru kujitawala.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa siku ya tarehe 9 Desemba mwaka 1961 wakati nchi yetu ikpata Uhuru huku jamaa zetu wa Zanzibar wakipata uhuru wao mwaka 1964 baada ya Mapinduzi yaliyowaondoa Watawala wa Kiarabu katika visiwa vya Unguja na Pemba. Nchi hizi ziliungana tarehe 26 Aprili 1964 na jina Tanzania kupatikana. 

Nachelea kusema kuwa hiyo ndiyo hali halisi ya Uhuru wetu, lakini kikubwa ninachokusudia kujadili katika makala haya ni namna ambavyo wananchi wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli za kuijenga nchi yao na kujiletea maaendeleo tokea nchi hizi zilipopata uhuru na kuungana.

Hapa ndipo inapoibuka dhana ya ugatuaji wa madaraka mikoani (kwa wananchi) ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa zilianzishwa ili kutekeleza na kukidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa lengo la kuwapa Wananchi uwezo wa kujiamualia masuala yao ikiwemo uchumi na kuinua hali za maisha .

Katika Ibara za 145 na 146 ya Katiba imetamkwa wazi kuwepo kwa vyombo vya wananchi ambavyo vitaanda mazingira wezeshi ya kupeleka madaraka kwa wananchi na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika kubuni, kupanga, kutekeleza na kusimamia mipango ya kijamii na kiuchumi Sera ya ugatuaji madaraka ya mwaka 1998 imesisitiza kuongeza uwezo wa kifedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe.

Ili kuimarisha Muungano wetu, Wizara zinazoshughulikia masuala ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika pande mbili za Muungano zimejiwekea utaratibu wa kukutana katika Vikao vya Mashirikiano ambavyo hulenga katika kubadilishana uzoefu katika utendaji wa sekta ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. 

Wakati Tanganyika inapata uhuru wake ilikuwa na majimbo kumi ya Utawala ambayo yalirithiwa toka utawala wa kikoloni wa Kiingereza. Mwaka 1966, Rais wa Awamu ya kwanza Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwa Mamlaka aliyopewa, aliunda Mikoa 15 na kuondokana na utaratibu wa mgawanyo wa nchi katika Majimbo. 

Madhumuni ya kuanzishwa kwa maeneo haya ni kusogeza huduma za kijamii na kiutawala karibu zaidi na wananchi. Kwa upande wa Serikali za Mitaa, Serikali iliendelea na mfumo wa Serikali za Mitaa iliourithi kutoka kwa wakoloni na kuutumia kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya kidemokrasia. 

Kutokana na changamoto mbalimbali zilizoukabili utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa mara baada ya uhuru na mwanzoni mwa miaka ya sabini, Serikali ilizifuta Mamlaka hizi mwaka 1972 na kuanzisha Mfumo wa Madaraka Mikoani. 

Mfumo huu ulizifanya Serikali za Mitaa kuitegemea Serikali Kuu kwa kila jambo. Kutokana na wananchi kutoshiriki katika maamuzi na pia katika shughuli za maendeleo, uchumi wa nchi ulididimia na viwango vya maisha kushuka.
Kutokana na hali hii, Serikali za Mitaa kwa upande wa Mamlaka za Miji zilirejeshwa tena mwaka 1978 na mwaka 1984 Serikali za Mitaa upande wa Mamlaka za Wilaya pia zilirejeshwa.

Ili kuziimarisha na kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizi ni kuanzishwa kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulioanza mwaka 1998 ambao ulilenga katika kupeleka madaraka kwa wananchi. 

Dhana ya Upelekaji wa Madaraka kwa Wananchi imeelezwa kwa kina zaidi katika Sera ya Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1998.

Katika Sera hii, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapewa uhuru wa kufanya maamuzi mbalimbali yahusuyo utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika Mamlaka zao na kuwashirikisha katika kujiletea maendeleo na ustawi wao kwa ujumla. Pamoja na kupewa uhuru huo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuutumia kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi na endapo zitakwenda kinyume chake, Serikali Kuu inao wajibu wa kikatiba na kisheria kuingilia kati na kuchukua hatua stahili dhidi ya Mamlaka hizo. 

Mfumo huu umeonyesha mafanikio katika nyanja za usimamizi wa fedha, raslimali watu, ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa pamoja na mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Ni kutokana na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kulikoleta mafanikio makubwa katika kuongeza fursa za elimu ya msingi na kupitia mipango ya maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari (MMEM na MES).

Aidha, kutokana na shule hizi kuwa katika kila Kata nchini, mwaka 2008 Serikali ilihamishia majukumu la usimamizi wa shule za Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuyaweka chini ya TAMISEMI wakati huo ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. 

Ni jukumu letu kulinda mafanikio haya na kukabiliana na changamoto ambazo zimejitokeza katika kipindi hiki. Katika kutambua nafasi ya Serikali za Mitaa katika kuleta maendeleo ya wananchi, mwaka 2005 Serikali iliamua kwamba kila ifikapo tarehe 1 Julai ya kila mwaka iwe ni kilele cha Siku ya Serikali za Mitaa nchini pote. Katika kipindi hiki, Serikali za Mitaa hupata muda wa kujitathmini pamoja na kueleza mafanikio iliyoyapata kwa Wananchi. 

Sherehe hizi hufanyika katika Halmashauri zote na kitaifa hufanyika katika Halmashauri ambayo huchaguliwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT). 

Tuendelee kuimarisha Sekta ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kutimiza matarajio ya wananchi hapa ndipo tunahitaji zaidi kutumia dhana ya Hapa Kazi Tu ili kila Mamlaka itimize wajibu wake kwa ukamilifu kwa kutumia fursa zilizopo kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI George Boniphace Simbachawene anasema kuwa Sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ilianzishwa kwa lengo la kushirikisha wananchi katika hatua mbalimbali za kujiletea maendeleo ikiwa ni njia ya kuwafanya wawe ni sehemu ya maendeleo yao wenyewe.

Simbachawene anasema kuwa kutokana na sera hiyo Serikali imetenga maeneo mapya ya kiutawala ili kusogeza karibu zaidi hadi 30, machi 2016 takribani wilaya sita (6) zimeanzishwa na ikiwemo Mkoa mpya wa Songwe,
Anasema kuwa wilaya zilizoanzishwa kuwa ni pamoja na  Wilaya za Songwe (Songwe), Kigamboni (Dar es Salaam), Ubungo (Dar es Salaam),  Malinyi (Morogoro), Tanganyika(Katavi), Chalinze (Pwani), na Itigi (Singida).

Katika mgawanyo huo pia zimeanzishwa mamlaka za Serikali za Mitaa za Halmashauri za miji za Ifakara (Morogoro), Bunda (Mara), Mbulu (Manyara),Kondoa (Dodoma), Newala (Mtwara) pamoja na Mbinga (Ruvuma).
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2016 Tanzania bara ina mikoa 26, Wilaya 139, Halmashauri 181, Tarafa 562, Kata 3,963, Mitaa 4,037, Vijiji 12,545 pamoja na Vitongoji 64,677.

“Lengo la kuanzisha maeneo haya ya kiutawala ni kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi na kuongeza kasi ya maendeleo,” alisema Simbachawene.

Katika kuhakikisha kunakuwepo na ufanisi katika utekelezaji wa dhana hiyo Waziri Simbachawene anasema kuwa Wenyeviti wa Mitaa, Vijijini na Vitongoji hawana budi kutambua kuwa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi pamoja na mambo mengine inawahimizia viongozi hao kutoa taarifa za mapato na matumizi ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila baada ya miezi mitata kama kinavyoainishwa kwa mujibu wa sheria.

Dhana hiyo inataka uwepo uwazi katika kutoa taarifa ili kukidhi matakwa ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji miongoni mwa jamii zetu jambo ambalo linapunguza kama siyo kuondoa kabisa kero za wananchi.

Katika moja ya ziara za kikazi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewahi kunukuliwa akisema kuwa wajibu wa viongozi wa Serikali za Mitaa ni kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua huku huko kwani zipo Mamlaka kamili zenye wajibu wa kuhudumia wananchi na siyo kusubiri mpaka waje katika ngazi za juu.

Anasema kuwa ngazi hizo za madaraka zimeanzishwa ili kurahisisha namna bora ya kuwahudumia wananchi, ambapo wapo viongozi kuanzaia ngazi ya Kitongoji hadi Manispaa na Majiji yote hiyo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma katika maeneo hayo ya kiutawala.

“Sitegemei kuona wananchi wanakuja kwangu kuleta kero zao nawaagiza mfanye kazi karibu na wananchi uwepo wenu nyinyi kama viongozi si wa bahati mbaya; utaratibu huu ulianzishwa mahususi ili kusogeza huduma kwa jamii ili waweze kujiletea maendeleo, hivyo mshirikiane vizuri naamni kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanikiwa,” anasema Makonda.
Wadau mbalimbali wanaeleza kuwa Sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi ni nzuri na imesaidia sana katika kuharakisha maendeleo katika maeneo yao kwani inawapa fursa ya kushirirki katika kubuni, kupanga na kufanya maamuzi ya utekelezaji wa miradi ya maenedeleo katika maeneo yao.

Alex Assenga, mkazi wa mtaa wa Mwongozo, kata ya Makuburi jijini Dar es Salaam anasema kuwa katika mtaa wao dhana ya ugatuaji wa madaraka imekuwa na tija kiasi kwamba wananchi bila kujali itikadi zao, ushirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

“Sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ni jambo jema sana kwani inawafanya wananchi kuwa sehemu ya chimbuko la miradi ya maenedeleo katika maeneo yao, na kusisitiza kuwa dhana hiyo inaongeza hamasa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza na kusimamia miradi hiyo,” alisema Asenga.

Anasema kuwa ongezeko la Shule za msingi na Sekondari katika maeneo mbalimbali ya nchi ni moja ya matokeo chanya ya utekelezaji wa sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kwani wananchi walishirikishwa katika ujenzi wa shule hizo na kweli waliitikia na kufanikisha ujenzi huo.

Kutokana na umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa karibu, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamuwa kuirejesha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa chini ya Ofisi ya Rais ili kuraishisha ufuatiliaji utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi kwa karibu zaidi.

Pamoja na mambo mengine Serikali kuu imeongeza usimamizi wa karibu zaidi ili kuziba mianya ya rushwa kwa kusimamia mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa ikiwemo baadhi ya tozo kuahimshiwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  nah ii imesababishwa zaidi na ubadhirifu uliokuwa umekidhiri hapo awali.

Sera ya ugatuaji madaraka ya mwaka 1998 imesisitiza kuongeza uwezo wa kifedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe. Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 imeainisha vyanzo vya mapato kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Mikopo ni miongoni mwa vyanzo hizo.

No comments