Serikali yajipanga Kuhakikisha Sekta ya Kilimo Inatoa Mchango Zaidi katika kufikia nchi ya Uchumi wa Viwanda
Mwambawahabari
SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imesema kuwa imeandaa mikakati mbalimbali ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inatoa mchango zaidi katika kufikia nchi ya uchumi wa kati.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa kwa ushirikiano wa Idara ya Habari – MAELEZO na kituo cha televisheni cha TBC, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Dkt. Florence Turuka alisema kuwa Serikali imeandaa mikakati hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili viwanda viweze kupata malighafi, chakula cha kutosha pamoja na ajira kwa wananchi.
“Serikali imeamua kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mazao kwa ajili ya soko, kushirikisha sekta binafsi katika kuongeza thamani ya mazao, ili kuvutia wakekezaji katika sekta ya kilimo nchini” alisema Dkt. Turuka.
Kwa mujibu wa Dkt. Turuka alisema ili kuhakikisha huduma za ugani zinakua za kisasa Serikali inadhamiria kutumia simu za mkononi zitakazorahisisha utoaji wa taarifa kwa wataalamu wa kilimo, ikiwa ni pamoja na kusaidia wakulima kupata huduma za kitaalamu kwa wakati.
Aidha Dkt. Turuka alisema mikakati mingine inayotekelezwa na Serikali ni pamoja na kuongeza idadi ya matrekta hadi kufikia 6,000 badala ya 400 yaliyokuwepo awali.
Aliongeza kuwa Serikali imekusudia pia kujenga maghala karibu na maeneo yanayozalisha mazao ya matunda na mbogamboga ili kuweza kuyahifadhi kwa muda kabla mazao hayo hayajapekelekwa sokoni ili kupunguza uharibifu.
Naye Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mathew Mtigumwe alisema Serikali itaboresha mfumo wa takwimu wa wataalamu wa kilimo pamoja na kuwajengea uwezo ili kusaidia utekelezaji wa maendeleo ya kilimo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali inawakaribisha wawekezaji wa kilimo cha miwa ambapo imeandaa zaidi ya hekta 6000 kwa ajili ya kilimo hicho nchini.
Post a Comment