Ads

PSPF WATOA RAI KWA WAJASIRIAMALI KUJIUNGA NA MPANGO WA HIARI.



Na Jacquiline Mrisho 
mwambawahabari
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) umetoa rai kwa wajasiriamali kujiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari ili kuweza kupata huduma ya hifadhi ya jamii.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Uendeshaji wa mfuko huo, Hadji Jamadary wakati wa uzinduzi wa maonesho ya kwanza ya viwanda vya Tanzania uliofanyika katika viwanja vya sabasaba jijini humo.


Jamadary amesema kuwa mpango huo utawawezesha wananchi wasio na ajira rasmi kupata fursa ya huduma ya hifadhi ya jamii kama wapatavyo wanachama wenye ajira rasmi  pia unawawezesha wanachama walio katika mfuko huo kuweza kujiwekea akiba ya ziada.

“Mpango huu wa hiari ni mfuko ulio huru ambao unamruhusu mwananchi yoyote mwenye umri kuanzia miaka 18, mwenye uraia wowote hata kama anafanya kazi ndani au nje ya nchi, hivyo tunawaomba wananchi wote kuchangamkia fursa hii kwa manufaa ya maisha yao ya baadae,”alisema Jamadary.

Ameongeza kuwa hadi sasa mfuko una jumla ya wananchi 98,733 ambao tayari wamejiunga na mfuko huo lakini kwa kutambua umuhimu wa mfuko huo zaidi ya wananchi 102 wameshajiunga wakati maonyesho hayo yanayotarajiwa kumalizika mnamo Disemba 11 mwaka huu yakiendelea.

Aidha, Afisa huyo ametaja jumla ya mafao 6 yaliyopo katika mfuko huo yakiwemo ya elimu, ujasiriamali, uzee, kifo, ugonjwa au ulemavu, matibabu na fao la kujitoa pia mfuko huo unatoa fursa kwa mwanachama kukopa nyumba na viwanja.

Kuhusiana na fao la matibabu, Jamadary amefafanua  kuwa mwanachama atapatiwa bima ya afya yenye gharama ya shilingi 76,800 kwa mwaka mzima pia ataruhusiwa kuwaingiza wategemezi watano ambapo kila mmoja atalipiwa kiasi hicho cha fedha kwa mwaka mmoja.

Mpango wa hiari umeanzishwa mwaka 2013 ukiwa na lengo la kupanua wigo wa uanachama kwa kuandikisha wananchi waliojiajiri au kuajiriwa  katika sekta rasmi au isiyo rasmi.

No comments