Ads

MIPANGO BORA YA MATUMIZI YA ARDHI HULETA MAENDELEO – DR. KUSILUKA.



Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari
Ukuaji wa nchi na maendeleo yake huchangiwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi unaotekelezwa na wananchi hasa wale wanaohusika katika shughuli za ujenzi wa miundombinu.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dr. Moses Kusiluka alipokuwa akifungua rasmi Kongamano na Mkutano Mkuu wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Ardhi lililofanyika katika viwanja vya chuo hicho.


Dr. Kusiluka amesema kuwa ni muhimu kwa taifa kutazama mipango ya matumizi ya ardhi kama mbinu moja wapo itakayochochea maendeleo ya nchi, hivyo ametoa rai kwa kila mwananchi kulitilia mkazo suala hilo ili kuhakikisha nchi inapiga hatua za kimaendeleo.

“Kama zilivyo hatua nyingine za maendeleo ya nchi zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa basi mpango bora wa matumizi ya ardhi pia ni sehemu isiyotakiwa kutengwa katika hatua za kukuza nchi,”alisema Dr. Kusiluka.

Dr. kusiluka amekipongeza chuo hicho kwa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii katika kuboresha sekta ya ardhi pamoja na sekta ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambao watakuja kuwa wataalam wazuri kwa siku zijazo.

Kwa upande wake Rais wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Baraza la Wahitimu wa Chuo hicho, Haruna Masebu amesema kuwa lengo la kuanzshwa kwa kongamano pamoja na baraza hilo ni kutafuta pesa kwa ajili ya kufanyia kongamano, kuandika machapisho yanayohusiana na maudhui yanayofundisha katika chuo hicho pamoja na kutumika kama daraja linalowaunganisha wahitimu waliomaliza miaka ya nyuma pamoja na waliopo sasa katika chuo hicho. 

“Mada inayojadiliwa katika kongamano hili inahusu ardhi, haki za ardhi, usawa pamoja na maendeleo yake ambapo majadiliano hayo yanalenga kuwajengea uelewa wahitimu hao katika kukuza na kuboresha sekta nzima ya ardhi na ujenzi kwa ajili ya kukuza maendeleo ya nchi nzima,” alisema Masebu.

Baraza hilo linalofanyika kila mwaka limeanzishwa tangu Disemba 12 mwaka 2012 na inakadiriwa kuwa na wanachama zaidi ya 500, ili kukuza kongamano linalosimamiwa na Baraza hilo ni lazima kila mwanachama kuchangia shilingi 20,000 ya ada ya uanachama pamoja na shilingi 50, 000 ya ada ya mwaka. 
                                    

No comments