Ads

MHANDISI GISSIMA MKURUGENZI MPYA WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA).



Na Daudi Manongi
mwambawahabari
Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imemteua Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala Dk.Lutengano Mwakahesya aliyestaafu mwezi Juni 2016.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Dk.Gideon Kaunda inaeleza kuwa uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya mwaka 2005 ya Nishati Vijijini katika kikao kilichofanyika Tarehe 17 Desemba 2016.

Aidha taarifa hiyo inaeleza kuwa kabla ya uteuzi huu Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Imeongeza kuwa Mhandisi Gissima ana uzoefu wa miaka 20 katika Sekta ya Nishati na pia ameshika nyadhifa mbalimbali tangu mwaka 2008 alipoajiriwa REA.

Mbali na hayo Mhandisi huyu amehitimu Shahada ya Uhandisi katika fani ya Umeme, Shahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Uhandisi,Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA) zote kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Stashahada ya Juu ya Sheria na Upatanishi na Usuluhishi ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam.

Bodi ya Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) inaomba sekta mbalimbali kumpatia ushirikiano Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-Hanga ili kumuwezesha  kutekeleza majukumu na malengo yake.

No comments