WIZARA YA HABARI YAPOKEA VIFAA VYENYE THAMANI ZAIDI YA SH.MILIONI 20 KUTOKA UBALOZI WA CHINA NCHINI.
Na Shamimu Nyaki-WHUSM.
mwambawahabari
Ubalozi wa China nchini umeipatia Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo vifaa vya ofisi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 ikiwa ni kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Serikali hizo mbili.
Hatua hiyo imekuja ikiwa na lengo la kusaidia katika kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa ambayo katika mpango wa miaka mitano ya maendeleo ya Serikiali inatakiwa kuongeza ajira pamoja na pato la taifa kupitia kazi mbalimbali za sanaa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo leo Jijini Dar es Salaam Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw. Petro Lyatuu aliushukuru Ubalozi huo kwa mchango wao wa kuhakikisha sekta ya sanaa inakuwa na kuleta mabadiliko nchini.
“Tunashukuru Ubalozi wa China kwa kutupatia vifaa hivi ambavyo vitasaidia sana utendaji katika Sekta ya Sanaa ambayo inaendelea kukua kwa kasi hapa chini na kusaidia kuimarisha ushirikiano mzuri baina ya Serikali yetu na China”Alisema Bw. Petro Lyatuu.
Naye Mshauri wa masuala ya Utamaduni kutoka Ubalozi huo Bw Gao Wei amesema kwamba China itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara katika kuendeleza Sanaa kwa kutoa misaada mbalimbali kwa kadri itakavyohitajika.
“Tutaendelea na ushirikiano huu sio tu kwa kutoa msaada wa vifaa bali pia kubadilishana uzoefu na taaluma ya Sanaa ili Sekta hii ikue na kuheshimika na kutambulika rasmi kama ajira ”Alisema Bw Gao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bibi Leah Kihimbi amesema kuwa vifaa hivyo vitaimarisha utendaji kazi wa Sekta ya Sanaa ukizingatia kuwa ni Sekta ambayo imebeba dhamana kubwa ya kutangaza Sanaa ndani na nje ya nchi.
Vifaa vilivyotolewa na Ubalozi wa China ni pamoja na Komputa 4,Komputa Mpakato 1,Kamera ya video moja na Luninga vyote vikiwa na jumla ya dhamani zaidi ya milioni 20.
Post a Comment