MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI KUWANUFAISHA JAMII
Na Lorietha Laurence-WHUSM
mwambawahabari
Mnamo tarehe 16 Septemba mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliwasilisha kwa mara ya kwanza Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari Bungeni Mjini Dodoma.
Tangu kuwasilishwa kwa Muswada huo kumekuwa na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau habari ni kwa namna gani jamii na tasnia ya habari na itanufaika na Sheria hiyo.
Mmoja wa wadau wa habari Bw. Malekela Maingu katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii alihoji endapo Muswada huu upo kwa ajili ya kunufaisha wanahabari peke yake, swali ambalo wadau wengi watakuwa wakijiuliza.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari upo kwa ajili ya watu wote kwa kuwa katika Muswada huo umezingatia kumlinda mwandishi na mwananchi kwa kutoa habari za uhakika ili kuzuia mgawanyiko kwa jamii endapo itatokea kashfa.
Katika sehemu ya Tano kifungu cha 32(1) cha Sheria hii inaeleza kuwa jambo lolote kama likichapishwa au kutangazwa linaweza kuharibu sifa ya mtu kwa kumfanya achukiwe, adharauliwe au afanyiwe kejeli au linaweza kumharibia mtu kazi yake kwa kuchafua jina lake au kumvunjia heshima yake jambo hili litahesabika kuwa ni kashfa.
Kufuatia kifungu hicho ni wazi Sheria hii itasimamia haki ya mtu endapo taarifa zitakazotolewa kuhusu mtu huyo zitabainika kuwa ni za uongo zenye nia ya kumchafulia jina ama kumdhalilisha.
Kifungo hicho kinaendelea kueleza kuwa Sheria hii inamtaka mwandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi kwa kutoa taarifa zilizo za kweli na zenye uhakika ili kulinda maslahi ya nchi na watu wake.
Naye Bw. Amour Kagya ameipongeza Serikali kwa kuleta Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari na kueleza kuwa kupitia Sheria hii kazi ya uandishi wa habari itaheshimiwa na kuthamaniwa.
Bw. Kagya amesema wanahabari watanufaika kwa uwepo wa mfuko wa mafunzo ya habari kwani utawasaidia kujiendeleza na kukuza tasnia ya uandishi wa habari hivyo kuipa hadhi fani hiyo.
Post a Comment