Tanzania yapewa tuzo za ustawi wa jamii na ushirikishaji wa wanawake katika mkutano wa AU
Na. Immaculate Makilika
mwambawahabari
mwambawahabari
Serikali ya Tanzania
imepewa tuzo 2 za masuala ya Ustawi wa Jamii pamoja na ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi
ya maamuzi ya Serikali na Taasisi mbalimbali katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU) uliofanyika hivi
karibuni Kigali nchini Rwanda.
Hayo yamesemwa leo na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi, Augustine
Mahiga, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
salaam kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa 27 wa Umoja wa nchi za
Afrika uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.
“Tanzania imetambuliwa na AU kama nchi ambayo
kwa miaka 15 sasa imekua na mikakati mbalimbali
ya kitaifa ya kuzingatia haki za
wanawake na kutimiza malengo ya Milenia,”
alisema Balozi Mahiga.
Aliongeza kuwa
Tanzania ni kati ya nchi tano bora katika bara la Afrika ambazo zimepewa tuzo
hizo.
Katika hatua
nyingine, Balozi Mahiga amasema kuwa katika mkutano huo wa 27 viongozi wa
Afrika walizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo hati ya kusafiria Afrika (passport), ambayo
itawezesha watu wa bara hilo kusafiri katika nchi zote za Afrika.
Balozi Mahiga
aliongeza kuwa, lengo la kuanza kutumia hati hiyo ya kusafiria kwa nchi za Afrika
ni kutoa vikwazo vilivyokuwepo wakati wa kutembelea na kusafiri ndani ya nchi
hizo.
Aidha, Balozi Maiga amesema
kwamba, kutolewa kwa hati ya kusafiria ya Afrika ni ishara ya Umoja na
mshikamano, hati hizo zimeanza kutolewa kwa marais na viongozi wa Serikali wa nchi
ambazo zilihudhuria mkutano huo. Hati hizo zitatumika kwa kuzingatia sheria za
kila nchi.
Hali kadhalika, mkutano
huo ulijadili migogoro ya nchi za Burundi na Sudani Kusini ambapo viongozi hao
walikubaliana kupeleka Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Sudani Kusini ili
kutenganisha majeshi ya pande mbili zinazoendelea kupigana nchini humo.
Aidha, mgogoro wa
Burundi bado unaendelea kupatiwa ufumbuzi kutokana na jitihada mbalimbali
zinazoendelea kufanywa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye aliteuliwa na mapema
mwaka huu na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano wa 27 wa
Umoja wa nchi za Afrika wenye wanachama 54 ulifanyika Kigali nchini Rwanda tarehe
18 mwezi huu, ukiwa ni mkutano wa pili kwa mwaka huu ulikua na kauli mbiu
inayosema mwaka wa haki za binadamu.
Post a Comment