Ads

MKURUGENZI WA ADO AFUNGUKA MAZITO MUSWADA WA SHERIA VYAMA VYA SIASA.

Mkurugenzi Mtendaji wa Alliance for Development Organization (ADO) Bw. Habibu Mchange akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Wanasiasa nchini wametakiwa kuunga mkono muswada wa sheria wa vyama vya siasa jambo ambalo litasaidia kuepuka uonevu ndani ya vyama pamoja kutumia fedha za ruzuku kinyume na taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Alliance for Development Organization (ADO) wakati akitoa maoni yake kuhusu muswaada wa kisheria ya vyama vya siasa Bw. Habibu Mchange, amesema kuwa muswada huu ni rafiki kutokana unakwenda kutatua changamoto za vyama vya siasa hapa nchini.

Amesema kuwa muda mrefu wanasiasa wamekuwa wakilalamika kuhusu mambo yanayofanyika ndani ya vyama ikiwemo utaratibu wa kutumia fedha za ruzuku ambazo ni kodi za watanzania.

"Muswada huu wa sheria wa vyama vya siasa unakwenda kutatua changamoto zote, muda mrefu nilikuwa tunalalamika sasa tunapata majibu" amesema Bw. Mchange.

Bw. Mchange ambaye ni mwanasiasa amesema kuwa 
mswaada huo wa kisheria unapinga ufisadi katika vyama vya siasa pamoja na kuleta ufanisi katika utendaji wa vyama hivyo.

Bw. Mchange amefafanua kuwa kuna utaratibu ambaoumekuwa ukifanyika wa kuchagua wabunge wa viti maalumu ambao sio rafiki katika vyama vya siasa.

"Ni vizuri vyama vya siasa kuunga mkono muswada wa sheria vyama vya siasa kutokana ni rafiki na unakwenda kusimamia mambo muhimu ikiwemo matumizi ya ruzuku" amesema Bw. Mchange.

Amesema kuwa kupitia muswada huo kisheria msajili wa vyama vya siasa ataweza kusimamia sheria hiyo, kitu ambacho kutakuwa na uwazi katika matumizi ya fedha pamoja na mambo mengine yanayofanyika katika vyama vya siasa.

Hata hivyo hivi karibuni vyama 10 vya  upinzani nchini Tanzania kupitia muungano wao vimefungua kesi Mahakamani Kuu ya Tanzania kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa kujadiliwa na Bunge kwa ajili ya kuupitishwa kuwa sheria. 

Akisoma tamko la umoja huo  Alhamisi Januari 03, 2019, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa  muswada huo unakinzana na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 hivyo ni muhimu kwao kuupinga.

“Tumefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar chini ya hati ya dharura kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kujadiliwa na Bunge kwa minajiri ya kuupitisha kuwa sheria kwa sababu unakinzana na katiba ya nchi" alisema.

Kabwe alisema kuwa muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na Mamlaka ya Usimamizi (Regulatory Authority), kuwa na mamlaka ya kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha/ kumfukuza mtu uanachama.

No comments