TRA YAKUSANYA TRILIONI 15.5 KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Mwamba wa habari
Makusanyo ya kodi kwa Mwaka wa
Fedha wa 2017/18 yameongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 15.5 kutoka
shilingi trilioni 14.4 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 sawa na ongezekeo la asilimia
7.5.
Akizungumza leo jijini Dar es
Salaam wakati akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi ya mwaka wa fedha 2017/18,
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Bw. Richard Kayombo amesema kuwa katika mwezi Juni, 2018 pekee, TRA imekusanya
jumla ya shilingi trilioni 1.5 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.4 kwa
mwezi Juni, 2017 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 8.0.
“TRA inapenda kuwapongeza na
kuwashukuru walipakodi wote ambao mchango wao umeiwezesha Serikali kupata
mapato haya tunayotangaza leo kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za
maendeleo na za jamii zikiwemo ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara,
ununuzi wa ndege, upatikanaji wa elimu, afya na mambo mengine kwa manufaa ya
watanzania wote,” alisema Kayombo.
Kayombo amezitaja sababu
zilizosababisha kuongezeka kwa makusanyo hayo kuwa ni pamoja na elimu ya kodi
kuzidi kueleweka kwa
walipakodi na wananchi kwa ujumla, kuongeza ukaribu na walipakodi kwa kuwasikiliza
na kutatua changamoto zao za kikodi, kuongezeka kwa walipakodi wapya kupitia
kampeni ya kuwasajili kwa kuwafuata waliko na kurahisisha ulipaji wa kodi kwa
njia ya kielektroniki.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kuwa, katika Mwaka huu wa Fedha 2018/19,
TRA imedhamiria kutekeleza kwa vitendo kampeni kabambe ya msamaha wa riba na
adhabu kwa malimbikizo ya madeni ya nyuma na inategemea kuongeza urahisi wa
kulipa madeni ambayo yalikuwa kikwazo kwa wafanya biashara wengi kulipa na hata
kuendelea na biashara.
“Vilevile, mamlaka imedhamiria kuongeza kasi ya usajili wa
walipakodi wapya. Hivyo, tunaendelea na kasi ya utambuzi na usajili wa
wafanyabiashara wadogo ili kila mtu anayestahili kulipa kodi asajiliwe na kuchangia
kikamilifu maendeleo ya Taifa,” alieleza Kayombo.
Mkurugenzi
Kayombo ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kuendelea kulipa kodi kwa
hiari na kujenga utamaduni wa kudai Risiti za Kielektroniki za Kutolea Risiti
(EFDs) kila mfanyabiashara anapofanya mauzo na mnunuzi anatakiwa kudai risiti
kila anaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Post a Comment