Mfumuko wa Bei Washuka na Kufikia Asilimia 3.8.
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Aprili, 2018
umepungua hadi kufikia asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.9 ilivyokuwa
mwezi Machi, 2018.
Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei
za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2018 imepungua
ikilinganishwa na mwezi Machi, 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii
kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim
Kwesigabo amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Aprili, 2018
kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Aprili
kumechangiwa na kushuka kwa gharama za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa
kipindi kilichoishia mwezi Aprili, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi
Aprili, 2017”, alisema Bw. Kwesigabo.
Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia
kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na mahindi kupungua kwa asilimia
5.2, unga wa mahindi umepungua kwa asilimia 5.6, mtama kwa asilimia
7.3, unga wa muhogo kwa asilimia 9.3, maharage kwa asilimia 9.2 na mihogo
mibichi kwa asilimia13.2.
Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei nchini
una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki
ambapo nchini Kenya mfumuko wa bei wa mwezi Aprili, 2018 umepungua hadi
asilimia 3.73 toka asilimia 4.18 mwezi Machi na nchini Uganda umepungua
hadi asilimia 1.8 toka asilimia 2.0 mwezi Machi, 2018
Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi
ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
Post a Comment