Makamu wa Rais ashauri kurasimishwa kwa Ajira zisizo rasmi.
Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabariblog
Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan ameshauri kurasimishwa kwa ajira zisizo rasmi ili ziweze kuchangia katika pato na maendeleo ya Taifa kwa kukuza uchumi wa mtu mmoja na wa Taifa kiujumla.
Ametoa ushauri huo Leo Jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika Mashariki na Kati amesema ili kuwezesha kuzalisha ajira nyingi ni vyema kurasimisha ajira zisizo rasmi ili kutoa nafasi nyingi kwa vijana kujiajiri na kuondokana na wimbi la ukosefu wa ajira barani Afrika.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria mkutano wa vyama vya mifuko ya Jamii Afrika Mashariki na kati wakiwa wamesimama kumuaga mgeni rasmi Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua mkutano huo leo Jijini Dar es Salaam.
“Ili wananchi waweze kujiamini na maisha yao ya baadae ni lazima wawe na imani na ajira zao pamoja na hali nzuri ya kiuchumi,kukua kwa uchumi ndio njia rahisi inayowezesha upatikanaji wa ajira.”
“Kuanzishwa kwa Mifuko ya Jamii kumesaidia kuwainua wananchi kiuchumi,kijamii na inawalinda watu wasipoteze ajira zao, na ndio sababu Mifuko hii inajulikana kama “haki kwa watu wote” (Universal Right)” Alisema Mhe. Samia.
Ameongeza kuwa, ni lazima iundwe mikakati mizuri ya kukuza uchumi ambayo itasaidia katika ukuzaji wa biashara,uwepo wa bajeti yenye nguvu,kuwekeza katika miundo mbinu pamoja na kuwa na mifumo mizuri ya kodi.
Aidha,amewaomba wanaohusika na utungaji wa sera za Mifuko ya Jamii kuzingatia sera zinazochochea ukuaji wa uchumi.
Mkutano huu ulihudhuriwa na Mawaziri na Manaibu Waziri kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati ,Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ,wakurugenzi wa mabenki na wawakilishi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Post a Comment