Rais Magufuli Atekeleza Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda La Kuhakiki Silaha Upya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amekuwa mtu kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la
kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya Shortgun na Pistol
zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha
zoezi la uhakiki wa Silaha, na ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha
nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za
kukabiliana na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu ili kutokomeza kabisa
vitendo hivyo.

"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa
silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na
wewe una silaha?" Amehoji Rais Magufuli
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
salaam Kamishna Simon Sirro, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono zoezi
hilo na amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika
kwa mafanikio.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea
kiti cha Umeya katika Jiji la Dar es salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata
Meya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala ya
kuendelea kurumbana.
Dkt. Magufuli amesema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo
ya uchaguzi huo, ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya
kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde
kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio
demokrasia ya kweli" ameongeza Rais
Magufuli
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiiweka silaha yake
vizuri mara baada ya kuhakikiwa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Post a Comment